Thursday, 1 October 2015

Chakula Bora

Unga wa dona kwa mchicha...

Kila Mtu anaweza kula chakula bora!
Ugali wa dona na mchicha ni maandalizi ya chakula cha bei nafuu mno…lakini ni miongoni mwa chakula bora.


Unga wa dona ulioandaliwa vizuri huwa una faida nyingi sana zaidi ya hata unga ambao umekobolewa. Faida hizo ni za kiuchumi au hata za kiafya. 

Faida ya Matumizi ya Unga wa dona

Kiuchumi:
1.      Ukisaga mahindi bila ya kukoboa unapata unga mwingi kwa kila kilo utakayoisaga. Hii ni kwa sababu ukoboaji wa mahindi kunapoteza kiasi fulani cha unga na virutubisho pia.
2.       Uandaaji wa mapishi ya unga wa dona ni rahisi zaidi katika ngazi ya familia.
Kiafya:
Katika Unga wa dona kuna kiasi kikubwa cha mafuta, protini, madini, vitamini, na nyuzinyuzi (fibre). Kwahiyo, unaimarisha zaidi lishe ya mlaji.

Faida za kula Mchicha(Kwa uchache)


1.      Huboresha mfumo wa Kinga mwili
2.     Huboresha uwezo wa kuona

3.     Huboresha mfumo wa akili na nevu (nervous system)

Thursday, 20 August 2015

vyakula vinavyoimarisha afya ya ngozi

 Kula chakula chenye virutubisho sahihi ni jukumu la lazima la binadamu ili kuwa na afya njema. Dunia ina vyakula vya asili ambavyo ndani yake kuna virutubisho muhimu vinavyosaidia mwili kupambana na magonjwa na pia kuimarisha afya. Vyakula hivyo ni vile vya kijani ambavyo vina uwezo mkubwa zaidi katika kuponya magonjwa na kusaidia pia kukarabati, kujenga mwili na kuimarisha siha.                       
 Ngozi nayo ni sehemu muhimu ya mwili ambayo ina jukumu kubwa la kuukinga na kuufunika mwili na viungo mbalimbali na afya yake ni jambo la kuzingatiwa. Aina za vyakula tunavyopendelea kula vinaweza kuchangia katika muonekano wa ngozi zetu.
 Kuna aina za vyakula vinavyosaidia katika kutunza ngozi yako bila gharama kubwa. Bi Samatha Heller mtaalamu wa lishe katika Chuo Kikuu cha Tiba cha New York City anasema kuwa, kila tunachokula kinakuwa sehemu ya mwili wetu na kila tunapo vyakula bora ndivyo ngozi zinavyoonekana vizuri. Naye Elein Linker mtaalamu wa biokemikali na mwasisi wa kituo cha kutunza ngozi cha DDF anasema, matatizo mengi ya ngozi kama vile chunusi ya aczema (ngozi kuwa nyekundu,kuvimba,kuwasha au ukavu) itching and dryness  yanaweza kuwa yanahusiana na lishe. Hivyo tunashauriwa kujitahidi kufuata kanuni za afya ili kuufanya mwili uwe na afya nzuri kwa kula chakula bora, kufanya mazoezi, kupumzika kwa muda mrefu, vivyo hivyo ngozi nayo inatakiwa kutunzwa vyema kupitia lishe.


  Asali ambayo hutengenezwa na nyuki kwa viambato asilia ni chakula muhimu kwa ajili ya kuimarisha afya ya ngozi na pia afya ya binadamu. Sababu kubwa ya kutumia mafuta ya kuipaka ni kuifanya ngozi iwe na unyevu nyevu. Asali husaidia kutunza na kuhifadhi unyevu kwenye ngozi na ina kiwango kikubwa cha sukari na asidi ambazo huzuia vijidudu wanaozaliana kwenye ngozi. Vyakula vingi vya baharini pia vina kiwango kikubwa cha Zinc na Omega 3 ambazo ni muhimu kwa siha ya ngozi. Faida za Omega 3 ni pamoja na kuondoa kukakamaa au ukavu wa ngozi, kupunguza kuvimba na kukunjamana kwa ngozi na husaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini hivyo kuboresha ngozi.
 Kiini cha yai kina vitamini A na B huku sehemu yenye ute ikiwa na protini nyingi ambayo ni muhimu pia kwa ngozi . Mada ya Tretinoin inayopatikana kwenye Vitamin A husaidia kuondoa chunusi na mikunjo ya ngozi. Mada nyingine ya Biotin inayopatikana kwenye Vitamin B ni muhimu kwa afya ya ngozi na kucha na protini inayopatikana kwenye ute wa yai ni muhimu katika kuifanya ngozi iwe nyororo na yenye kung'aa na pia husaidia ngozi kujilinda vizuri na mionzi ya jua.



 Matunda yenye vitamini C kama vile chungwa, limao na mengineyo ni muhimu pia katika kuimarisha afya ya ngozi, kwa sababu husaida kutengeneza collagen, ambayo ni aina ya protini inayotengeneza ngozi. Vitamini C inasaidia kuondoa uvimbe na mikunjo ya ngozi na hivyo kuilinda ngozi isizeeke mapema.
Mboga za majani pia ni muhimu kwa afya ya ngozi kama tujuavyo zimesheheni vitamin na virutubisho vya aina mbalimbali vyenye faida kubwa kwa ngozi na mwili kwa ujumla.

Chanzo cha habari: Mitandao 

Wednesday, 19 August 2015

Ugonjwa wa Kipindupindu

  Kipindupindu ni miongoni mwa magonjwa ambayo husababishwa na aina ya bakteria aitwaye Vibrio cholerae, bacteria huyu husababisha mtu kuhara majimaji yenye rangi kama maji ya kupikia mchele. Ugonjwa huu ni wa kuambukizwa kwa njia ya viini vinavyoenezwa kupitia kwa kinyesi kutoka kwa wagonjwa wenye Kipindupindu.Mlundikano wa taka na maji ma chafu  pia ni moingoni mwa vyanzo vya Kipindupindu.


                                                                                                   
Mlundikano wa uchafu ndiyo chanzo cha Kipindupindu
Miongoni mwa hatua za msingi katika kujikinga na maambukizi ya kipindu pindu ni kunawa mikono wakati wowote kabla ya kutayarisha au kula chakula, kusafisha vyombo kama sahani, vikombe n.k. Nawa mikono kabisa kwa sabuni – kiganja, upande wa nyuma wa mkono, katikati ya vidole na kucha kwa sekunde baada ya kwenda haja na kabla ya kula na kuwa na akiba ya maji yaliyochemshwa pasipo na maji safi ya bomba.
Chanzo cha Habari: Mtandao wa intaneti

Saturday, 25 July 2015

Machungwa na zabibu hupunguza hatari ya kupata kiharusi

    Chuo cha Tiba cha Norwich huko Anglia Mashariki Uingereza, kimetafiti na kuangalia faida za matunda chachu (Citrus Fruit) pekee, kwa  mara ya kwanza tofauti na tafiti nyingi zinazo angalia umuhimu wa matunda na mboga za majani kwa afya kiujumla. Utafiti huu umehusisha maelfu ya wanawake lakini wataalamu wanaamini faida hizo za machungwa na zabibu pia zinapatikana kwa wanaume. Wataalamu hao wamechunguza umuhimu wa kemikali aina ya flavonoids ambayo ni jamii ya antioxidant (mada zinazoua kemikali hatari mwilini) inayopatikana katika matunda, mboga za majani na chokoleti nyeusi.


Utafiti huu uliochapishwa katika Jarida la Tiba la Kiharusi umesema kuwa, mada hiyo hupatikana kwa asilimia 82 kwenye machungwa na juisi ya machungwa, na hupatikana kwa asilimia 14 kwenye zabibu na juisi ya zabibu. Hata hivyo watafiti hao wamesema kwamba, kwa wale wenye kusudio la kuongeza kiwango kikubwa cha flavanones itawalazimu kula tunda asili la chungwa kwa wingi na si juisi za machungwa zinazotengenezwa kiwandani kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha sukari katika juisi hizo. Flavanones hutoa kinga dhidi ya kiharusi kutokana na kuongeza ufanisi wa mishipa ya damu kwenye ubongo na kutokana na kuwa na uwezo wa kuzuia maambukizi mwilini. 

 Lakini ni vyema tukawa makini pia kuwa matokeo ya utafiti huu yasiwafanye watu kuacha kula matunda ya aina nyingine pamoja na mboga za majani kwani nayo yana faida kubwa katika mwili wa binadamu. Pia tukumbuke kuwa, inawezekana kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi kama mtu atakula lishe bora iliyo na virutubisho vyote muhimu, kula matunda na mboga za majani kwa wingi, kufanya mazoezi mara kwa mara, kupunguza kiwango chumvi tunachokula, (kwani watu wenye asili ya Afrika wana kiashiria cha asili kinachojulikana kama salt retention gene ambacho hufanya kiwango kidogo cha matumizi ya chumvi mwilini kionekane kikubwa na hivyo kuongeza hatari ya kupata kiharusi), kupunguza uzito, kupunguza kiwango cha matumizi ya mafuta katika chakula, kulala masaa ya  kutosha na kupunguza msongo wa mawazo.

Tuesday, 23 June 2015

Maana ya neno SIHA (Afya)

 Kwa mujibu wa  ufafanuzi uliotolewa na kutangazwa na Shirika la Afya Duniani WHO katika mkutano wake wa tarehe 19-22 Juni 1946 na kusainiwa na wawakilishi wa nchi 61 duniani, 'afya ni hali ya mtu kuwa vizuri kimwili, kiakili na kijamii na sio tu kutokuwa na ugonjwa au udhaifu(Health is a state of complete physical, mental and social well-being and not merely the absence of disease or infirmity).' Ufafanuzi huo ulianza kutumika Aprili mwaka 1948 na hadi hii leo maana hiyo ya afya haijabadilika. Ufafanuzi huo unamaanisha kwamba, tunaposema mtu ana afya sio tu tunakusudia kuwa mwili wake hauna maradhi, upungufu au udhaifu bali pia mtu huyo anatakiwa asiwe na matatizo ya kimwili, kiakili na hata kijamii. 

Matunda yanayo boresha mfumo wa KINGA YA MWILI

Katika kipindi hiki cha hofu ya corona ni muhimu sana kuhakikisha kinga yako ya mwili iko juu muda wote. Lakini pia ni vizuri katika maisha...